Wahajiri zaidi ya elfu 3 wakamatwa Libya
Serikali ya Libya imewatia mbaroni maelfu ya wahajiri haramu katika mji wa Sabratha, kaskazini magharibi mwa nchi, ikiwa ni katika jitihada za kupambana na magendo ya binadamu.
Bassem Ghrabli, kamanda wa kikosi cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya amesema wahajiri haramu wapatao 3,150 wamekamatwa katika mji huo ambao ni moja ya vituo vya kuwasafirisha wahamiaji haramu kueleka barani Ulaya.
Amesema wamefanikiwa kuvunja mtandao huo wa magendo ya binadamu baada ya jitihada na mapambano ya karibu wiki tatu.
Wizara ya Afya ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya imesema makabiliano hayo yamesababisha watu karibu 40 kuuawa, wengine 300 kujeruhiwa, huku shule na hospitali za eneo hilo zikiharibiwa. Aidha vituo vya kihistoria vilivyoanishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) vilivyoko yapata kilomita 70 magharibi mwa mji mkuu Tripoli vimeharibiwa pia katika mapigano hayo.
Kamanda huyo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya ameongeza kuwa, aghalabu ya wahajiri hao wana asili ya Afrika, Uarabuni na Asia.
Mji wa Sabratha uligeuka kituo kikuu cha kuwasafirisha wahajiri haramu katika nchi za Ulaya toka mwaka 2011, baada ya kuuawa mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, Kanali Muammar Gaddafi.