Watu wenye silaha wawafyatulia risasi waandamanaji jijini Nairobi, Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35439-watu_wenye_silaha_wawafyatulia_risasi_waandamanaji_jijini_nairobi_kenya
Habari kutoka Kenya zinaarifu kwamba watu wenye silaha wamefyatua risasi dhidi ya mamia ya waandamanaji wa upinzani waliokuwa wanaelekea zilipo ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2017 11:25 UTC
  • Watu wenye silaha wawafyatulia risasi waandamanaji jijini Nairobi, Kenya

Habari kutoka Kenya zinaarifu kwamba watu wenye silaha wamefyatua risasi dhidi ya mamia ya waandamanaji wa upinzani waliokuwa wanaelekea zilipo ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) jijini Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

Maandamano hayo ni katika mfululizo wa malalamiko ya wapinzani wanaotaka kutekelezwa mabadiliko katika kukaribia uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu. Hakuna taarifa kamili iliyotolewa juu ya uharibifu uliosababishwa na shambulizi hilo, kama ambavyo pia haijabainika ikiwa shambulizi hilo lilifanywa na maafisa usalama wa serikali au la. James Orengo, mmoja wa viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA amewaonya wawakilishi wa chama tawala juu ya hatua yao ya kupasisha muswada wa marekebisho ya sheria za uchaguzi. Hayo yanajiri katika hali ambayo kamisheni ya haki za binaadamu nchini Kenya (KNCHR) imetangaza kuwa, hadi sasa jumla ya watu 37 waliuawa katika machafuko ya tangu tarehe 9 Agosti hadi tarehe 15 ya mwezi huo.

Baadhi ya waandamanaji

Taarifa iliyotangazwa Jumatatu ya leo na kamisheni hiyo imeongeza kuwa, katika machafuko hayo, watu wengine 126 walijeruhiwa. Taarifa hiyo imefafanua kuwa, vifo hivyo vilitokea katika maeneo ya Kawangware, Mathare, Kibra, Lucky Summer, Baba Dogo na Huruma-allin yote ya jiji la Nairobi. Aidha kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wengine waliuawa katika maeneo ya Kondele, Manyatta, Nyamasaria na Nyalenda katika kaunti ya Kisumu. Wapinzani nchini Kenya wanataka kufanyike marekebisho kadhaa kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio huku wakitishia kususia uchaguzi huo ikiwa matakwa yao hayatotelekezwa.