Mripuko wa lori lililotegwa bomu waua watu 40 mjini Mogadishu, Somalia
Polisi ya Somalia imetangaza kuwa watu wapatao 40 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya lori lililotegwa bomu kuripuka katika eneo lenye msongamano wa watu katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.
Kwa mujibu wa polisi, akthari ya waliouawa na kujeruhiwa katika mripuko huo ni raia wa kawaida.
Kapteni wa jeshi la Polisi Mohamed Hussein amevieleza vyombo vya habari kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vikilifuatilia lori hilo wakati liliporipuka katika eneo la Hodan yalipo maduka, hoteli, mikahawa na ofisi kadhaa za serikali. Amesema wanaamini lori hilo lilikuwa limelenga kushambulia hoteli katika eneo hilo.
Japokuwa hadi tunaingia mitamboni hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo lakini kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab lenye mfungamano na mtandao wa Al-Qaeda limekuwa likihusika na utegaji mabomu na mashambulio mengi ya kigaidi ya aina hiyo ndani ya Somalia na katika nchi jirani.../