Serikali Somalia yawaomba raia wachangie damu, waliouawa wapindukia 300
Serikali ya Somalia imetoa wito kwa wananchi kuchangia damu kwa ajili ya kutibu majeruhi wa shambulizi la kigaidi la Jumamosi iliyopita mjini Mogadishu ambalo limeua mamia ya raia wasio na hatia.
Waziri wa Habari wa Somalia, Abdirahman Omar Osman amesema Somalia haina benki ya damu na kwamba mapungufu ya mfumo wake wa huduma za afya yanatatiza jitihada za kutoa matibabu kwa mamia ya majeruhi wa shambulizi hilo.
Waziri Omar Osman amesisitiza kuwa, Somalia inahitajia damu na misaada ya kutambua maiti za watu waliouawa kwa ajili ya kukabidhiwa maiti kwa familia na jamaa zao.
Waziri wa Habari wa Somalia amesema maiti za zaidi ya watu mia moja ambazo hazikuweza kutambuliwa zilizikwa jana na kuongeza kuwa anatarajia maiti za waliosalia zitatambuliwa na kukabidhiwa kwa jamaa zao.
Mlipuko wa Jumamosi iliyopita uliofanywa kwa kulipua lori lililokuwa limetegwa bomu katikati ya mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, umetajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Somalia. Hadi sasa zaidi ya watu mia tatu wameripotiwa kufariki dunia katika shambulizi hilo la kigaidi ambalo maafisa wa serikali ya Somalia wanasema linafanana sana na yale yanayofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab.