Wahajiri haramu 147 waokolewa katika pwani ya Libya
Kikosi cha ulinzi katika pwani ya Libya kimesema kuwa kimewaokoa wahajiri haramu wa Kiafrika 147 katika eneo la pwani la Garabulli magharibi mwa nchi hiyo.
Askari usalama wa Libya wamesema kuwa baada ya kuokolewa, wahajiri hao haramu walipelekwa katika vituo vya kikosi cha majini huko Tripoli kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kitiba na kisha walihamishiwa katika vituo vya kuwahifadhi wahajiri haramu. Wahajiri hao haramu wa Kiafrika wameokolewa katika eneo la pwani la Garabulli magharibi mwa Libya.
Taasisi moja ya Ulaya inayohusika na Uokoaji wa Wakimbizi katika bahari ya Mediterrania kwa jina la "SOS Mediterranee" jana ilitangaza kuwa mapigano yanayoendelea huko Libya yamezidisha mgogoro wa kibinadamu katika bahari ya Mediterrania na kwamba maisha ya maelfu ya wahajiri ambao wanataka kuelekea Ulaya kwa kuvuka bahari hiyo wakikimbia mapigano huko Libya, wako katika hali ya hatari. Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa pia imeitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua haraka iwezekanavyo kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoisibu Libya na kuwapokea wakimbizi zaidi.