Chama cha Jubilee chawashitaki viongozi wa NASA kwa kuwashawishi Wakenya kususia uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35817-chama_cha_jubilee_chawashitaki_viongozi_wa_nasa_kwa_kuwashawishi_wakenya_kususia_uchaguzi
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubelee nchini Kenya, Raphael Tuju amesema kuwa uongozi wa chama hicho umewasilisha kesi katika Mahakama ya Juu ambayo iliagiza uchaguzi wa urais urudiwe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2017 01:13 UTC
  • Chama cha Jubilee chawashitaki viongozi wa NASA kwa kuwashawishi Wakenya kususia uchaguzi

Katibu Mkuu wa Chama cha Jubelee nchini Kenya, Raphael Tuju amesema kuwa uongozi wa chama hicho umewasilisha kesi katika Mahakama ya Juu ambayo iliagiza uchaguzi wa urais urudiwe.

Akizungumza na waandishi wa habari Alkhamisi ya jana Tuju amesema: “Tunataka viongozi wa NASA waliowataka wafuasi wao kutoshiriki uchaguzi ulioagizwa na Mahakama ya juu waadhibiwe kwa kukaidi agizo la korti.” Mwisho wa kunukuu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Jubelee nchini Kenya, Raphael Tuju

Katika nyaraka za keshi zilizowasilishwa, Jubilee inadai kuwa viongozi wa NASA wamekuwa wakiandaa maandamano na kuzua ghasia nchini Kenya kuchochea wananchi wasishiriki uchaguzi wa marudio. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Jubelee nchini Kenya, Rais Kenyatta ameapa kutoshiriki mazungumzo yoyote na upinzani kuhusu masuala ya marudio ya uchaguzi na kwamba, uchaguzi huo utafanyika katika tarehe iliyopangwa yaani tarehe 26 mwezi huu. Aidha amesisitiza kuwa, mzozo kuhusu uchaguzi wa urais unapaswa kusuluhishwa na Mahakama ya Juu pekee. Kadhalika kiongozi huyo wa chama tawala amepuuzilia mbali mwaliko wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, aliyetaka kukutana na Rais Kenyatta.

Kiongozi wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga

Akizungumzia suala hilo, Tuju amesema: “Ikiwa Chebukati ana tatizo kuhusiana na maandilizi ya uchaguzi, anafaa kwenda mahakamani na si vinginevyo”. Hayo yanajiri katika hali ambayo jioni ya jana kiongozi wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga alikutana na Wafula Chebukati, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika kikao ambacho hata hivyo kilisusiwa na Rais Uhuru Kenyatta.