Helikopta yaanguka Kenya, wanachama wa Jubilee wanaaminika kuaga dunia
Ndege moja aina ya helikopta imeanguka katika ziwa Nakuru nchini Kenya muda mfupi baada ya kuondoka katika hoteli moja mjini humo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga ya ya Kenya, Gilbert Kibe amethibitisha kuwa ndege hiyo ya helikopta ilianguka muda mfupi baada ya kupaa ikitokea katika Hoteli ya Jarika County Lodge.
Helikopta hiyo ilikuwa katika kampeni za uchaguzi wa rais wa marudio uliopangwa kufanyika baadaye wiki hii.
Mkurugenzi wa Idara ya Taifa ya Kukabiliana na Majanga, Pius Mwachi amesema kuwa, juhudi za uokoaji zilikuwa zikiendelea kwa ajili ya kupata watu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo ingawa vyombo vya dola vinasema kuwa, kuna uwezekano mdogo wa kupata manusura.
Habari zinasema watu waliokuwa katika ndege hiyo walikuwa wanachama wa chama tawala cha Jubilee.
Watu walioshuhudia ndege hiyo ikiondoka katika Hoteli ya Jarika County Lodge wanasema ilikuwa ikipaa chini chini kabla ya kuanguka.
Mkurugenzi wa Idara ya Taifa ya Kukabiliana na Majanga Pius Masai amesema kuwa ndege ya polisi imetumwa katika eneo hilo kusaidia juhudi za uokoaji.