Waziri: Wanajeshi 12 wa Niger wameuawa katika shambulizi
(last modified Sun, 22 Oct 2017 07:36:59 GMT )
Oct 22, 2017 07:36 UTC
  • Waziri: Wanajeshi 12 wa Niger wameuawa katika shambulizi

Waziri wa mambo ya Ndani wa Niger ametangaza habari ya kuuawa wanajeshi 12 wa nchi hiyo katika shambulio jipya lililotokea kwenye mpaka wa nchi hiyo na Mali, kaskazini magharibi mwa Niger.

Mohamed Bazoum ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kuna shambulio jipya limetokea. Wanajeshi 12 wameuawa. Serikali ya Niger imeanza mara moja kuwasaka watu waliofanya shambulizi hilo.

 

Shambulio hilo la jana limetokea baada ya lile la mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba ambalo liliua wanajeshi wanne wa Marekani na wanajeshi wanne wa Niger katika mpaka wa nchi hiyo na Mali. Eneo hilo limekuwa likishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha.

Shambulizi la jana alfajiri limetokea katika mji wa Ayorou katika eneo la Tillaberi, kilomita 200 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Niger, Niamey.

Maafisa usalama wamesema kuwa, watu walioshambulia walifika kwenye eneo hilo wakiwa ndani ya magari matano na baadaye kukimbia baada ya polisi wa kuongeza nguvu kufika katika eneo hilo. Habari hiyo imeongeza kuwa, wanavijiji wamewaona wanamgambo hao wakiondoka na miili ya watu waliouawa.

Tags