Watu 10 wauawa 16 wajeruhiwa katika shambulizi jipya nchini Somalia
Mripuko wa bomu la kutegwa ardhini na ufyatulianaji risasi baina ya askari wa AU na wanamgambo wa al Shabab umeua watu wasiopungua 10 na kujeruhi wengine 16 kusini mwa Somalia.
Maafisa usalama wa Somalia wametangaza leo Jumatano kwamba gari lililokuwa limewabeba askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) limeripukiwa na bomu karibu na mji wa Afgoye, kusini mwa Somalia na kuzusha mapigano yaliyopelekea watu wasiopungua 10 kuuawa na wengine 16 kujeruhiwa.
Maafisa hao wamesema kuwa tukio hilo limetokea katika eneo lililoko baina ya Arbiska na Lafole, karibu na mji wa Afgoye ulioko umbali wa kilomita 30 kusini mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Maafisa hao wameliambia shirika la habari la Xinhua kwa njia ya simu kwamba wamepokea ripoti kuwa watu 10 wameuawa wengi wao wakiwa ni raia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya gari hilo la askari wa AMISOM kukanyaga bomu na baadaye kutokea ufyatulianaji risasi baina ya askari hao na genge la kigaidi la al Shabab.
Wiki iliyopita pia, kulitokea mashambulio makubwa sana ya mabomu mjini Mogadishu ambayo yaliua watu 358 na kujeruhi wengine 228.
Msemaji wa kikosi cha AMISOM, Wilson Rono amethibitisha kutokea shambulio hilo la leo na kusema kuwa, raia wengi wameuawa wakati askari wa AU walipokuwa wanavyatuliana risasi na wanamgambo wa al Shabab. Amesema, kikosi cha AMISOM kimepoteza askari mmoja na mwengine mmoja amejeruhiwa.
Hata hivyo duru za kujitegemea zimesema kuwa, askari wasiopungua watatu wa AU wameuawa pamoja na walimu wawili, wanafunzi kadhaa, mgambo mmoja na magaidi wasiopungua wanne wa al Shabab.