Uhuru aongoza katika matokeo ya uchaguzi wa marudio yaliyotolewa hadi sasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35974-uhuru_aongoza_katika_matokeo_ya_uchaguzi_wa_marudio_yaliyotolewa_hadi_sasa
Uhuru Kenyatta anaongoza katika matokeo ya uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika jana nchini Kenya huku matokeo yakiendelea kutolewa kutoka vituo mbalimbali vya uchaguzi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 27, 2017 01:21 UTC
  • Uhuru aongoza katika matokeo ya uchaguzi wa marudio yaliyotolewa hadi sasa

Uhuru Kenyatta anaongoza katika matokeo ya uchaguzi wa marudio wa urais uliofanyika jana nchini Kenya huku matokeo yakiendelea kutolewa kutoka vituo mbalimbali vya uchaguzi.

Matokeo yaliyotumwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) yanaonyesha kuwa Uhuru Kenyatta anaongoza kwa kura 442,052 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliyepata kura 6,321.  

Wakenya jana Alkhamisi walielekea kwenye masanduku ya kupigia kura katika uchaguzi wa marudio wa urais kufuatia kutenguliwa ule wa awali uliofanyika Agosti 8 mwaka huu. Mahakama ya Kilele ya Kenya ilitengua matokeo ya uchaguzi huo wa rais kwa hoja kwamba Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo (IEBC) ilifanya baadhi ya makosa katika mchakato wa uchaguzi. 

Tarehe Mosi Septemba Mahakama ya Kilele ya Kenya iliiamuru tume hiyo kuendesha uchaguzi wa marudio katika muda siku 60 kwa mujibu wa sheria. Muungano wa upinzani Kenya (Nasa) ulitangaza kujiondoa katika uchaguzi wa marudio wa jana ukisema kuwa IEBC imeshindwa kutekeleza marekebisho. Uchaguzi wa marudio wa jana uligubikwa na vurugu na ghasia katika baadhi ya ngome za muungano wa upinzani.

Wafuasi wa upinzani wakiwarushia polisi mawe huko Kibera Nairobi wakipinga uchaguzi wa marudio 

Nasa ilisema pia kwamba uchaguzi huo hautakuwa huru na wa uadilifu iwapo marekebisho wanayoyataka hayatatekelezwa. Odinga juzi aliwatolea wito wafuasi wake kususua uchaguzi huo wa marudio wa rais japokuwa Rais Uhuru kwa upande wake aliwatolea wito wapiga kura kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo.

Watu wasiopungua wanne wameuawa katika mkoa wa Nyanza na mji wa Machakos nchini Kenya katika ghasia za uchaguzi huo wa marudio wa rais.