Umoja wa Ulaya wataka kutatuliwa hitilafu za ndani nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36049-umoja_wa_ulaya_wataka_kutatuliwa_hitilafu_za_ndani_nchini_somalia
Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kupatiwa ufumbuzi hitilafu za ndani nchini Somalia ili kuboresha hali ya usalama wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa na hali ya mchafukoge.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2017 10:09 UTC
  • Umoja wa Ulaya wataka kutatuliwa hitilafu za ndani nchini Somalia

Umoja wa Ulaya umetoa wito wa kupatiwa ufumbuzi hitilafu za ndani nchini Somalia ili kuboresha hali ya usalama wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa na hali ya mchafukoge.

Catherine Ray, msemaji wa Umoja wa Ulaya amesema hayo katika radiamali yake kwa mashambulio ya hivi karibuni ya kigaidi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na kusisitiza juu ya udharura wa kutatuliwa hitilafu za ndani kwa ajili ya kuboresha hali ya usalama wa nchi hiyo.

Msemaji wa Umoja wa Ulaya ameongeza kuwa, kuweko mazungumzo baina ya viongozi wa serikali ya Somalia  na viongozi wa kieneo yatapelekea kuongezeka amani na uthabiti katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Itakumbukwa kuwa, watu wasipoungua 25 waliuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa baada ya gari lililokuwa limetegwa bomu kulipuka nje ya hoteli mashuhuri katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu siku ya Jumamosi.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Aidha katikati ya mwezi huu watu karibu 360 waliuawa katika hujuma za kigaidi zilizoulenga mji wa Mogadishu, katika hujuma iliyotajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Somalia.

Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianzisha mashambulizi yake nchini Somalia mwaka 2006 ambapo kutokana na mashambulizi ya jeshi la serikali ya nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMlSOM, lililazimika kukimbia kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu na kuelekea maeneo mengine ya mbali.

Licha ya operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM kuonekana kupata mafanikio, lakini kundi hilo la kitakfiri lingali linadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.