UN yalaani mauaji ya mateka Libya, yataka uchunguzi ufanyike
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36054-un_yalaani_mauaji_ya_mateka_libya_yataka_uchunguzi_ufanyike
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya amelaani mauaji ya mateka wasiopungua 37 nchini humo na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu jinai hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2017 21:47 UTC
  • UN yalaani mauaji ya mateka Libya, yataka uchunguzi ufanyike

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya amelaani mauaji ya mateka wasiopungua 37 nchini humo na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu jinai hiyo.

Ghassan Salameh amesema kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kumefanyika jinai nyingi nchini Libya na kwamba viongozi wa nchi hiyo wanapaswa kuwafungulia mashtaka wahalifu na watu waliohusika na jinai hizo. 

Siku chache zilizopita liligunduliwa kaburi la umati lililokuwa na miili ya watu wasiopungua 37 katika viunga vya mji wa Benghazi nchini Libya. 

Maiti zilizogunduliwa katika kaburi hilo zilikuwa zimefungwa mikono kwa kamba na zilikuwa na alama za kupigwa risasi.

Maiti za mateka wasiopungua 37 zimegunduliwa katika kaburi la umati Libya

Kaburi hilo limegunduliwa katika eneo lisilokuwa na makazi ya watu katika kitongoji cha Abyar kinachodhibitiwa na wapiganaji wa Jenerali mstaafu, Khalifa Haftar.

Baadhi ya ripoti zinasema miili iliyokutwa katika kaburi hilo ni ya askari waliokuwa wakishikiliwa katika jela inayodhibitiwa na jeshi la Haftar tangu miezi kadhaa iliyopita.

Libya inasumbuliwa na machafuko makubwa ya kisiasa na kiusalama yaliyoanza baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi.