Rais wa Somalia atangaza azma imara ya kupambana na ugaidi
Rais wa Somalia ametangaza azma yake imara ya kupambana na magaidi katika nchi hiyo ambayo wiki za hivi karibuni imepoteza mamia ya watu katika mashambulio ya magaidi.
Rais Mohamed Abdullahi maarufu kama Farmajo ameashiria hujuma ya kigaidi ya siku ya Jumamosi katika mji mkuu Mogadishu na kusema, serikali yake ina irada imara ya kupambana kikamilifu na ugaidi.
Akizungumza Jumatatu wakati wa kongamano la usalama, alisema lazima kuwepo mpango maalumu wa kuunganisha vikosi vya kijeshi kote Somalia ili kaungamiza magaidi wakufurishaji wa al-Shabab.
Kauli hiyo imekuja baada ya watu 29 kuuawa baada ya gari lililokuwa limetegwa bomu kulipuka nje ya hoteli mashuhuri katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu siku ya Jumamosi.
Kundi la kigaidi la Al Shabab lilidai kuhusika na hujuma hiyo.
Hujuma hizo za Jumamosi zimetokea wiki mbili bada ya watu 350 kuuawa katika hujuma ya kigaidi mjini Mogadishu ambayo ilitajwa kuwa hujuma mbaya zaidi ya kigaidi kuwahi kushuhudiwa Somalia.
Magaidi wakufurishaji wa al-Shabab wanalenga kuipindua serikali ya Somalia na wamekuwa wakitekeleza hujuma nchini humo kwa muda mrefu.