Usafiri wasitishwa Mandera, Kenya baada ya hujuma ya magaidi wa Al Shabab
Hujuma ya kundi la kigaidi la Al Shabab katika Kaunti ya Mandera, kaskazini mashariki mwa Kenya imepelekea usafiri kusitishwa kwa muda wa siku tatu.
Wamiliki mabasi katika eneo hilo wamechukua uamuzi huo baada ya magaidi wakufurishaji wa al-Shabab kushambulia na kuteketeza magari mawili ya polisi aina ya Land Cruiser katika mji wa Daba, Kaunti ya Mandera Jumatatu usiku.
Magari hayo mawili yalikuwa yamewabeba maafisa 12 wa polisi ambao walikuwa wakisindikiza basi lililokuwa likielekea Mandera wakati yaliposhambuliwa kwa maguruneti yaliyorushwa kwa roketi. Hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha katika tukio hilo ingawa afisa mmoja wa polisi alijeruhiwa huku magaidi wakifanikiwa kutoroka baada ya hujuma yao.
Polisi wanasema shambulizi hilo ni la kwanza kuripotiwa baada ya utulivu wa miezi mitatu. Taarifa zinasema magaidi wa al-Shabab wameanza kujikusanya tena katika eneo hilo kutokana na mvua kubwa ambazo zinafanya iwe vigumu kushambuliwa.
Kundi la kigaidi la Al Shabab lenye makao yake Somalia mara kwa mara hutekeleza mashambulizi ndani ya ardhi ya Kenya kuishinikiza serikali ya nchi hiyo iondoe wanajeshi wake wanaohudumu katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM.