Wahajiri 73 wapoteza maisha katika fukwe za Libya
Wahajiri 73 wamekufa maji katika bahari ya Mediterranean wakati walipokuwa wanajaribu kuzifikia fukwe za Italia kutokea Libya.
Shirika la habari la IRNA limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mtumbwi uliokuwa umewabeba wakimbizi hao umepata ajali na kuzama karibu na fukwe za Tripoli, mji mkuu wa Libya.
Afisa mmoja wa Libya amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, walinzi wa fukwe za Libya wamefanikiwa kuwaokoa watu 47 tu wakiwemo wanawake 16 na watoto wadogo 30, lakini watu wengine wote waliokuwemo kwenye mtumbwi huo wamekufa maji.
Siasa za kupenda vita za nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati na katika baadhi ya nchi za Afrika zimewalazimisha mamilioni ya watu kukimbia nchi zao zilizovamiwa na machafuko na kutafuta usalama wa roho zao katika nchi nyingine.
Hata hivyo, huko wanakokimbilia nako hakuna usalama na wanakumbwa na matatizo chungu nzima. Nchi za Magharibi ambazo zinashutumiwa kuwa ndio wasababishaji wakuu wa matatizo ya nchi za wakimbizi hao, zimefunga mipaka yao na haziko tayari kuwapokea.
Libya nayo imetumbukia kwenye machafuko na ukosefu mkubwa wa usalama tangu mwaka 2011 wakati jeshi la nchi za Magharibi NATO lilipoivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika kampeni ya kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi.