Nov 10, 2017 14:45 UTC
  • Watu 10 wauawa katika shambulizi la ISIS eneo la Sinai, Misri

Kwa akali watu 10 wameuawa katika shambulizi la kundi la kigaidi lenye mafungamano la genge la kitakfiri la Daesh (ISIS) katika eneo la Sinai nchini Misri.

Duru za kiusalama zinasema kuwa, raia wanane na wanajeshi wawili wameuawa katika shambulizi hilo usiku wa kuamkia leo, baada ya wanachama wa kundi hilo kuuzingira msafara wa malori yaliyokuwa yamebeba saruji katika mji wa Nakhl, katikati mwa Peninsula ya Sinai.

Luteni Kanali Ibrahim Hussein Mohammed ni miongoni mwa maafisa wa jeshi la Misri waliouawa katika hujuma hiyo.

Wapiganaji wa genge hilo la kigaidi ambalo huko nyuma lilifahamika kama Ansar Beit al-Maqdis mbali na kutekeleza mauaji hayo, wametoweka na silaha za askari hao na kuteketeza moto malori saba ya kubeba saruji.

Wanajeshi wa Misri katika kituo cha upekuzi eneo la Sinai

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Oktoba, raia wanne waliuawa katika shambulizi la roketi la kundi hilo la ukufurishaji katika mji wa Arish, katika Peninsula ya Sinai nchini Misri.

Eneo hilo la kaskazini mwa Misri limekuwa uwanja wa mashambulizi ya makundi yenye silaha yenye mafungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh tangu mwaka 2013, baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani kwa nguvu Mohamed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.

Tags