Zaidi ya wakimbizi laki moja wamesharejea Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36317-zaidi_ya_wakimbizi_laki_moja_wamesharejea_somalia
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, zaidi ya wakimbizi laki moja wa Kisomali wamesharejea nchini kwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2017 04:14 UTC
  • Zaidi ya wakimbizi laki moja wamesharejea Somalia

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, zaidi ya wakimbizi laki moja wa Kisomali wamesharejea nchini kwao.

Taarifa ya shirika hilo imesema, wakimbizi laki moja na 8,498 wa Kisomali wamesharejea nchini humo tangu mwezi Disemba 2014 hadi hivi sasa.

Hata hivyo shirika hilo limelalamika kwamba, hali mbaya ya misaada ya kibinadamu na kuongezeka ukosefu wa usalama katika maeneo ya mpaka wa Kenya na Somalia pamoja na gharama za kuwahamisha wakimbizi hao ni vikwazo vikubwa katika zoezi la kuwarejesha nyumbani wakimbizi wa Somalia.

Wanamgambo wa al Shabab wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Somalia

 

UNHCR aidha limesema, maafisa wa shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa Mataifa wanawasaidia tu wakimbizi wa Kisomali ambao wanataka kurejea nyumbani kwa hiari.

Mgogoro wa Somalia umeshapelekea watu milioni mbili kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo. Sehemu kubwa ya wakimbizi hao wako katika nchi jirani ya Kenya.

Kwa miongo mitatu sasa Somalia imekuwa ikishuhudia fujo, mauaji na mashambulizi ya kila namna. Katika kipindi chote hicho, Somalia imekuwa ikiendeshwa bila ya serikali kuu yenye nguvu. Umoja wa Afrika unaisaidia serikali dhaifu ya hivi sasa ya nchi hiyo kulinda usalama ingawa bado mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab yanaendelea kuripotiwa mara kwa mara katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.