Tume ya Kimataifa yapinga madai ya Saudia kuhusu mzingiro wa Yemen
Tume ya kimataifa iliyoundwa na Umoja wa Mataifa imefichua kwamba Saudi Arabia inazuia kwa makusudi misaada ya kibinadamu inayotumwa kwa watu wanaozongwa na maradhi na njaa huko Yemen na kutangaza kuwa, tume hiyo haikubali sababu zilizotolewa na utawala wa Riyadh za kuendelea kuizingira nchi hiyo.
Tovuti ya Marekani ya The Intercept imefichua kwamba, tathmini hiyo ya tume ya Umoja wa Mataifa ilitumwa katika waraka wa siri kwa wanadiplomasia tarehe 10 mwezi huu wa Novemba na kusema kuwa, wanachama wa tume iliyoteulwia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamethibitisha kuwa hawakupata ushahidi wowote unaounga mkono madai ya Saudi Arabia inayosema wapiganaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen wamepata makombora ya balestiki kutoka nje ya nchi, suala ambalo linakiuka maazimio ya kimataifa.
Wataalamu wa tume hiyo ya Umoja wa Mataifa wameongeza kuwa, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika mshambulizi dhidi ya watu wa Yemen unajaribu kutumia vibaya kifungu cha 14 cha azimio nambari 2216 kama kisingizio cha kuzuia misaada ya kibinadamu kwa watu wanaosumbuliwa na njaa na maradhi nchini Yemen.
Kifungu hicho kinazitaka nchi wanachama kuzuia uingizaji, uuzaji na kuingizwa bidhaa za kijeshi kwa wapiganaji wa Yemen.
Awali Mkurugenzi wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock alisema kuwa, mzingiro wa pande zote wa Saudi Arabia na washirika wake unaozuia kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Yemen unatishia maisha ya mamilioni ya raia wa nchi hiyo.
Maelfu ya raia wa Yemen wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizim kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo.