Waziri wa Masuala ya Dini wa Somalia afutwa kazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36835-waziri_wa_masuala_ya_dini_wa_somalia_afutwa_kazi
Hassan Ali Khayre, Waziri Mkuu wa Somalia amemfuta kazi Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo bila kutangaza sababu ya uamuzi wake huo.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Nov 26, 2017 10:33 UTC
  • Waziri wa Masuala ya Dini wa Somalia afutwa kazi

Hassan Ali Khayre, Waziri Mkuu wa Somalia amemfuta kazi Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo bila kutangaza sababu ya uamuzi wake huo.

Taarifa zaidi kutokka Mogadishu mji mkuu wa Somalia zinasema kuwa, Hassan Ali Khayre, Waziri Mkuu wa Somalia amemfuta kazi, Iman Abdullahi Ali aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Dini wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inayokabiliwa na machafuiko. 

Aidha katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Somalia amemteua Mohamed Mursal Sheikh Abdirahman balozi wa zamani wa Somalia nchini Uturuki kuziba nafasi ya Waziri wa Ulinzi iliyokuwa wazi tangu Abdirashid Abdullahi Mohamed ajiuzulu.

Abdirashid Abdullahi Mohamed alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Ulinzi wa Somalia mwezi uliopita wa Oktoba kwa sababu za binafsi.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Kwa miongo mitatu sasa Somalia imekuwa ikishuhudia fujo, mauaji na mashambulizi ya kila namna. Katika kipindi chote hicho, Somalia imekuwa ikiendeshwa bila ya serikali kuu yenye nguvu. Umoja wa Afrika unaisaidia serikali dhaifu ya hivi sasa ya nchi hiyo kulinda usalama ingawa bado mashambulizi ya genge la kigaidi la al Shabab yanaendelea kuripotiwa mara kwa mara nchini humo.

Mgogoro wa Somalia umeshapelekea watu milioni mbili kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo. Sehemu kubwa ya wakimbizi hao wako katika nchi jirani ya Kenya.

Hivi karibuni, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilitangaza kuwa, zaidi ya wakimbizi laki moja wa Kisomali wamesharejea nchini kwao kwa hiari.