Watu 50 wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36961-watu_50_wauawa_katika_mapigano_ya_kikabila_sudan_kusini
Watu wasiopungua 50 wameripotiwa kuuawa leo huko Sudan Kusini baada ya kutokea mapigano ya kikabila katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2017 12:51 UTC
  • Watu 50 wauawa katika mapigano ya kikabila Sudan Kusini

Watu wasiopungua 50 wameripotiwa kuuawa leo huko Sudan Kusini baada ya kutokea mapigano ya kikabila katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Viongozi wa kieneo katika mji mkuu Juba wamewaambia waandishi wa habari kwamba, watu wasiopungua 50 wameuawa leo kufuatia mashambulio ya wanamgambo katika jimbo la Jonglei. Taarifa zaidi zinasema kuwa, shambulio hilo la leo ni mlolongo wa mashambulio na mapigano baina ya makabila hasimu katika jimbo hilo.

Duru za kiusalama za Sudan Kusini zimeeleza kuwa, wanawake 23 ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha katika shambulio hilo.

Wakimbizi wa Sudan Kusini wakiwa nchini Uganda

Dut Achuek, Waziri katika ofisi ya Rais amesema kuwa, akthari ya wahanga wa shambulio hilo ni raia ambao nyumba zao zilichomwa na mifugo yao kuporwa. Washambuliaji hao wanasadikiwa kuwa ni kutoka kabila la Murle na waliwalenga watu wa kabila la Dinka wanaoishi katika vijiji hivyo vilivyoko yapata kilomita 150 kaskazini mwa Bor, makao makuu ya jimbo la Jonglei.

Machafuko ya ndani Sudan Kusini yalianza mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Rick Machar kwamba amehusika na jaribio la kutaka kupindua serikali yake. Hivi karibuni, Riek Machar alipinga pendekezo lililotolewa na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini la kufanyika mazungumzo ya kitaifa na akauomba Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na jumuiya nyingine za kimataifa kubuni mpango mpya wa utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo na kusitisha alichokiita mauaji ya kimbari Sudan Kusini.