AMISOM: Kupunguzwa wanajeshi wa AU Somalia kutakuwa na taathira hasi
Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimeeleza wasi wasi wake kuhusiana na mpango wa kupunguza idadi ya wanajeshi wanaohudumu kwenye kikosi hicho.
Fransisco Madeira, Mkuu wa AMISOM ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, operesheni za kikosi hicho zitavurugika pakubwa iwapo wanajeshi wa Kiafrika wanaosimamia amani nchini Somalia wataondolewa, na wachache watakaobaki wasiongezewe silaha na kuimarishwa katika uwezo wa kiintelijensia. Amesema anatumai Umoja wa Mataifa utatafuta namna ya kufidia pengo litakaloachwa kwa kuondoa mamia ya wanajeshi Somalia.
Hivi karibuni kikosi cha AMISOM kilisema kimeanza kupunguza idadi ya askari wake nchini humo na kwamba kufikia Disemba 31, askari 1000 wa kikosi hicho watakuwa wameondoka katika ardhi ya Somalia.
Kikosi hicho ambacho kiliundwa kupitia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na chenye jumla ya askari 22 elfu wa Kiafrika kimekuwa kikiisaidia serikali ya Somalia kupambana na magaidi wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2007.
Wakati huo huo, Mohamed Abukar Islow, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia amenukuliwa na Reuters akisema kuwa: "Serikali inataka kuondolewa vikwazo vya silaha, ili vikosi vyetu vipate silaha za kijeshi za kutosha."
Somalia iliwekea vikwazo vya silaha na Umoja wa Mataifa mwanzoni wa miaka ya 90 baada ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini vikaondolewa kwa kiasi fulani mwaka 2013, ili kutoa mwanya kwa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika liweze kujizatiti kwa silaha.