Mpango wa kuwarejesha nyumbani wahajiri wa Morocco kutoka Libya kutekelezwa
Wahajiri 236 raia wa Morocco wiki ijayo wataanza kurejea nchini kwao.
Husni Abu Ayana Mkuu wa Kundi la Kusimamia Wahajiri haramu nchini Libya leo amesema kuwa maafisa husika wa nchi mbili za Libya na Morocco wamesaini makubaliano kwa lengo la kuwarejesha nchini wahajiri 236 wa Morocco ambao wanafanya mgomo wa kula katika kituo cha kuwahifadhia wahajiri huko Libya.
Wahajiri hao walianza kususia kula chakula tangu mwezi Novemba wakilalamikia kuchelewa kurudishwa nchini kwao. Abu Ayana ameongeza kuwa wawakilishi wa ubalozi wa Morocco nchini Libya wamekitembelea kituo kimoja cha kuwapokea wahajiri kilichoko katika mji mkuu Tripoli na kutekeleza hatua za maandalizi ya kuwarejesha makwao wahajiri waliopo katika kituo hicho.
Afisa huyo wa Libya amesema kuwa wahajiri hao watarejeshwa nchini kwao kwa msaada wa kujitolea wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri. Abu Ayana amesema kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu karibu wahajiri elfu 17 wameondoka Libya kwa hiari yao wenyewe ili kurejea katika nchi zao.
Raia wengi wa nchi za kaskazini mwa Afrika wanajaribu kuvuka Libya kupitia bahari ya Mediterania kwa lengo la kuingia katika nchi za Ulaya. Kuenea harakati za makundi ya kigaidi na kushadidi machafuko na mizozo ya kisiasa katika akthari ya nchi za Kiafrika ni jambo ambalo limepelekea kuongezeka wimbi la wahajiri.
Aidha ripoti zinaonyesha kuwa, akthari ya wahajiri wa Kiafrika wamekuwa wakiuzwa kama bidhaa katika masoko ya watumwa nchini Libya.