Jeshi la Somalia lamkamata waziri wa zamani, laua walinzi wake 5
Askari wa jeshi la Somalia wamemtia nguvuni waziri wa zamani na mgombea kiti cha rais wa nchi hiyo na kuua walinzi wake 5 baada ya kuvamia nyumba yake mjini Mogadishu.
Abdiasis Ali msemaji wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Somalia, amesema Abdirahman Abdishakur anakabiliwa na tuhuma za uhaini. Amesema kuwa, waziri huyo wa zamani amekamatwa kwa kibali cha Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Usalama wa Ndani na kwamba walinzi wake wameuawa katika mapigano makali na askari usalama. Abdishakur mwenyewe amejeruhiwa mkononi.
Abdirahman Abdishakur ambaye aligombea kiti cha rais wa Somalia katika uchaguzi uliofanyika mwezi Februari mwaka huu, ni mwanasiasa wa kambi ya upinzani na mkosoaji mkuu wa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed.
Uchaguzi mkuu wa mwezi Februari nchini Somalia ulipongezwa sana na wafadhili wa nchi za Magharibi na kutajwa kuwa unaweza kuwa jiwe la msingi la kuangamizwa makundi ya waasi na kurejesha amani nchini humo.
Hata hivyo mashambulizi na mauaji ya holela yameongezeka sana nchini Somalia katika miezi ya hivi karibuni mjini Mogadishu na katika meneo mengine ya Somalia.