UNHCR: Kundi la kwanza la wahajiri waliokuwa Libya wahamishiwa Italia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37971-unhcr_kundi_la_kwanza_la_wahajiri_waliokuwa_libya_wahamishiwa_italia
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, kundi la kwanza la wahajiri waliokuwa katika jela moja nchini Libya wamehamishiwa nchini Italia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2017 04:14 UTC
  • UNHCR: Kundi la kwanza la wahajiri waliokuwa Libya wahamishiwa Italia

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limetangaza kuwa, kundi la kwanza la wahajiri waliokuwa katika jela moja nchini Libya wamehamishiwa nchini Italia.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, ndege moja ya jeshi la Italia jana ililichukua kundi la kwanza la wahajiri 110 waliokuwa katika jela nchini Libya na kuwapeleka kusini mwa Roma.

Kundi hilo la wahajiri linajumuisha wanawake na watoto wadogo na walikuwa katika magereza yaliyoko chini ya usimamizi wa serikali ya Libya na kwamba, wahajiri hao ni raia wa Ethiopia, Eritrea, Somalia na Yemen.

Hii ni mara ya kwanza kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kuchukua hatua hiyo, ambayo imepongezwa na jumuiya mbalimbali za kieneo na kimataifa.

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa UNHCR

Ripoti za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR zinaonyesha kuwa, kuna wahajiri elfu 18 katika vituo na jela zilizoko chini ya usimamizi wa serikali ya Libya.

Jumuiya za kutetea haki za binadamu zimekuwa zikikosoa vikali hali mbaya wanayokabiliwa nayo wahajiri hao katika maeneo wanakoshikiliwa na kwamba, wamekuwa wakifanyiwa vitendo visivyo vya kibinadamu.

Serikali ya Italia imelazimika kuwapokea wahajiri hao kufuatia mashinikizo ya makundi na jumuiya za kutetea haki za binadamu. Imeelezwa kuwa wahajiri hao watapatiwa makazi ya muda na serikali ya Italia kabla ya kushughulikiwa matakwa yao.