Somalia yarejeshewa udhibiti wa anga yake baada ya miaka 26
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38253-somalia_yarejeshewa_udhibiti_wa_anga_yake_baada_ya_miaka_26
Somalia imerejeshewa mamlaka ya kudhibiti anga yake kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1991.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2017 04:40 UTC
  • Somalia yarejeshewa udhibiti wa anga yake baada ya miaka 26

Somalia imerejeshewa mamlaka ya kudhibiti anga yake kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1991.

Hii ni baada ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa nchi hiyo kuzindua Kituo cha Taarifa za Safari za Anga katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Abdulle mjini Mogadishu hapo jana. Uwanja huo wa ndege upo chini ya ulinzi mkali wa Kikosi cha Askari wa Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM. 

Mbali na Rais Farmajo na mwenzake wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Galmudug, Ahmed Dualle Geelle, uzinduzi huo ulihudhuriwa na mawaziri, wanadiplomasia, wakuu wa usalama na maafisa wa Shirika la Kimataifa la Safari za Anga ICAO.

Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia

Waziri wa Uchukuzi wa Somalia, Mohamed Abdullahi Salad Omaar amesema uzinduzi huo umefuatia hatua ya shirika la Umoja wa Mataifa la ICAO kukabidhi udhibiti wa anga kwa serikali kuu ya Mogadishu, baada ya miaka 26.

Anga ya Somalia imekuwa chini ya udhibiti wa mamlaka ya mpito iliyoundwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) na Shirika la Kimataifa la Safari za Anga ICAO tangu mwaka 1991, baada ya kuanguka utawala wa kidikteta wa Siad Barre.