Operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi mjini Benghazi, Libya zafikia tamati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38417-operesheni_za_kijeshi_dhidi_ya_magaidi_mjini_benghazi_libya_zafikia_tamati
Jeshi la Libya lililo mashariki mwa Libya limetangaza kwamba limehitimisha operesheni zake dhidi ya makundi ya kigaidi mjini Benghazi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 02, 2018 04:06 UTC
  • Operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi mjini Benghazi, Libya zafikia tamati

Jeshi la Libya lililo mashariki mwa Libya limetangaza kwamba limehitimisha operesheni zake dhidi ya makundi ya kigaidi mjini Benghazi.

Duru za jeshi mjini humo zimearifu kwamba, kikosi maalumu cha jeshi la nchi hiyo kilihitimisha operesheni zake Jumatatu ya jana na kwamba baada ya kuwafurusha wapiganaji wenye silaha, mji huo umerejea katika hali yake ya kawaida. Taarifa hiyo imeongeza kwamba, katika operesheni hizo za mwisho, magaidi kadhaa wameangamizwa kama ambavyo kumepatikana pia miili ya wanamgambo wenye silaha katika eneo hilo. Itakumbukwa kuwa, mwamko wa wananchi dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi, mwaka 2011 ulianzia mjini Benghazi.

Mji wa Benghazi ukiwa umeharibiwa kufuatia operesheni hizo

Aidha mji wa Benghazi ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Libya, umekuwa uwanja wa machafuko katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kupelekea umwagikaji damu mkubwa, kati ya askari wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar kwa upande mmoja na makundi ya kigaidi na yenye kubeba silaha kwa upande wa pili. Licha ya kufikiwa makubaliano ya amani kati ya makundi yenye uhasama nchini Libya chini ya Umoja wa Mataifa sambamba na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa hapo mwaka 2015, lakini taifa hilo la kaskazini mwa Afrika bado linashuhudia machafuko na mauaji.