Al-Shabaab yaua watu 5 kwa tuhuma za ujasusi Somalia
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda limewaua kwa kuwamiminia risasi watu watano kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya vyombo vya kiintelejensia vya Kenya, Somalia na Ethiopia.
Genge hilo la kitakfiri kupitia radio yake ya Andalus limethibitisha kutekeleza hukumu hiyo jana Jumatano katika mji wa Kurtunwarey eneo la Shabelle ya Chini.
Mamia ya wakazi wa mji huo wakiwemo wanawake na watoto wadogo wamelazimishwa kutizama watano hao wakiuawa hadharani kwa kumiminiwa risasi, huku wakiwa wamefungwa kwenye vigingi.
Hata hivyo jaji aliyesoma hukumu dhidi ya watuhumiwa hao hakutoa ushahidi wala ithibati yoyote dhidi yao.
Mapema mwaka jana, kundi hilo liliwaua kwa kuwakata vichwa watu wanne walioshukiwa kuwa majasusi, kusini mwa Somalia.
Kabla ya hapo, wazee wanane wa vijiji vya eneo la Galmudug nchini Somalia waliuawa kwa kukatwa vichwa na kundi hilo la kigaidi, eti kwa kuwashawishi wakazi wa maeneo hayo kutolipa kodi na 'zaka' wanazotozwa kwa nguvu na al-Shabaab.