Magaidi kadhaa waangamizwa al Arish, Misri
(last modified Mon, 08 Jan 2018 15:42:59 GMT )
Jan 08, 2018 15:42 UTC
  • Magaidi wa Daesh kaskazini mwa Misri
    Magaidi wa Daesh kaskazini mwa Misri

Duru za kiusalama za Misri zimetangaza habari ya kuuawa magaidi kadhaa katika opereseheni iliyofanywa na jeshi la nchi hiyo mashariki mwa mji wa al Arish, makao makuu wa jimbo la Sinai Kaskazini.

Duru hizo zimetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa Misri wamefanya operesheni maalumu katika eneo la mashariki mwa al Arish na kupambana na kikundi kimoja cha kigaidi na kufanikiwa kuangamiza magaidi wanane. Hata hivyo duru hizo hazikutoa maelezo zaidi kuhusiana na operesheni hiyo.

Msikiti ulioshambuliwa na magaidi wa Daesh nchini Misri

 

Eneo la kaskazini mwa Misri hususan mkoa wa Sinai Kaskazini umekuwa ni uwanja wa mashambulizi ya mangenge mbalimbali ya kigaidi likiwemo lile wa Wila ya Sinai la genge la wakufurishaji wa Daesh.

Mwishoni mwa mwezi uliopita yaani Alkhamisi ya tarehe 28 Disemba 2017, wanajeshi sita wa Misri waliuawa katika mkoa huo. Bomu la kutegwa ardhini liliripuka baada ya kukanywagwa na gari la jeshi lililokuwa likilinda doria katika mji wa Bir al-Abd, kaskazini mwa Rasi ya Sinai.

Msemaji wa Jeshi la Misri katika eneo hilo, Kanali Tamer el-Rifaai alithibitisha habari hiyo na kusisitiza kuwa, afisa mmoja wa ngazi za juu na wanajeshi watano waliouawa katika shambulizi hilo. Msemaji huyo alilazimika kutoa tamko hilo, baada ya kuenea habari kuwa ni makamanda wawili wa kijeshi ndio waliouawa.

Siku chache kabla ya hapo, vyombo vya sheria nchini Misri vilikuwa vimetekeleza hukumu ya kuwanyonga watu 15 waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama katika jimbo hilo la Sinai Kaskazini.

Tags