Kwa akali wahajiri 64 wa Kiafrika wafa maji katika pwani ya Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38713-kwa_akali_wahajiri_64_wa_kiafrika_wafa_maji_katika_pwani_ya_libya
Kwa akali wahajiri 64 wameripotiwa kufariki dunia baada ya kuzama maji katika bahari ya Mediterranean wakati wakielekea nchini Italia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2018 04:11 UTC
  • Kwa akali wahajiri 64 wa Kiafrika wafa maji katika pwani ya Libya

Kwa akali wahajiri 64 wameripotiwa kufariki dunia baada ya kuzama maji katika bahari ya Mediterranean wakati wakielekea nchini Italia.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Jumatatu ya jana lilitangaza kuwa, boti lililokuwa limewabeba wahajiri 150 lilizama katika pwani ya Libya baada ya kupata hitilafu ambapo katika ajali hiyo wahajiri 64 walifariki dunia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto na wanawake kadhaa ni miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo. Kufuatia tukio hilo Tommaso Fabri, mkuu wa timu ya madaktari wasio na mpaka nchini Italia amekosoa vikali siasa za uhajiri za serikali ya Roma na nchi nyingine za Ulaya katika kujaribu kuwazuia wahajiri hao.

Wahajiri wakijaribu kuogelea baada ya boti yao kuzama maji

Jumapili iliyopita kuliripotiwa habari ya kuzama maji wahajiri 25 katikka pwani ya Libya baada ya boti yao kuzama wakiwa katika safari ya kuelekea Ulaya. Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) zaidi ya wakimbizi elfu tatu waliaga dunia mwaka jana wakijaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, vifo ambavyo vingi vilitokea katika njia ya bahari kutoka Libya kuelekea Italia. Akthari ya wahajiri hao ni raia wa nchi za Kiafrika ambao wanataraji kupata maisha mazuri na ajira huko barani Ulaya.