Jaji Mkuu Kenya: Inasikitisha kuona masikini ndio wanaohukumiwa zaidi jela kuliko matajiri
Jaji Mkuu nchini Kenya David Maraga, ameonyesha masikitiko yake kwa kile alichosema kuwa, masikini ndio wanaokamatwa na kutupwa jela kulikoni matajiri.
Maraga aliyasema hayo Jumatatu ya jana na kuongeza kuwa, watu masikini hukamatwa kwa makosa madogomadogo kama vile kukosa leseni za kufanya biashara na kuzua ghasia, huku washukiwa wa makosa makubwa na matajiri wakiachiliwa huru baada ya kesi zao kutayarishwa vibaya. Kwa mujibu wa Jaji David Maraga, kesi nyingi za makosa makubwa huondolewa mahakamani au washtakiwa wake kuachiliwa huru kinyume cha sheria. “Inapofikia uhuru unanunuliwa badala ya kuhakikisha haki, hii inaenda kinyume na sababu ya kuwepo kwa wasimamizi wa haki,” alisema, Maraga.
Jaji mkuu huyo wa Kenya aliyeyasema hayo wakati akizindua kamati ya mageuzi ya haki katika kesi za uhalifu kupitia Mahakama ya Juu, aliwataka mahakimu kusimamia haki ipasavyo bila ubaguzi wala upendeleo kati ya wenyenacho na masikini. Maraga alisema, kuna haja ya kufanyia mageuzi mfumo wote wa utafutaji haki kwa dharura akisema kuwa mfumo huo umekuwa ukikumbwa na changamoto nyingi. Pia alisema mfumo uliopo kwa sasa hautilii maanani maslahi ya vijana na ndio maana vijana wengi hujipata wakivunja sheria katika juhudi za kutafuta riziki zao na kwamba asilimia 75 ya wanaoshikiliwa jela wana umri kati ya miaka 18 na 35. Kamati ya Taifa kuhusu Usimamizi wa Haki (NCAJ) itachunguza idara hiyo na kutoa mapendekezo yake ambayo yatatumiwa kuleta mageuzi katika mfumo wa kutafuta haki katika kesi za uhalifu nchini Kenya.
Aidha kamati hiyo inayosimamiwa na Jaji Grace Ngenye wa Mahakama Kuu ina wanachama kutoka mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, Mwanasheria Mkuu Githu Muigai, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru pamoja na majaji wengine.