Kenya yajadili njia za kupambana na hujuma ya silaha za kibaiolojia
Kenya inapanga mkakati wa kukabiliana na hatari ya silaha za kibiolojia kupitia uwekezaji katika miradi inayolenga kuimarisha hatua za usalama wa kibaiolojia nchini humo.
Katika mkutano ambao umefanyika mjini Nairobi kuhusu kujadili nafasi ya vyuo vikuu katika kuimarisha hatua za usalama wa kibailojia, watunga sheria na wasomi wamesema ufadhili mkubwa wa fedha kwa ajili ya utafiti, kujenga uwezo, na elimu kwa jamii ni muhimu kwa kuimarisha uwezo wa Kenya wa kukabiliana na mashambulizi yanayofanywa na vikundi mbalimbali vinavyohusiana na matumizi ya kemikali za sumu za kibaiolojia.
Roy Mugiira, mkurugenzi wa huduma za kiufundi katika Tume ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu amesema vyuo vikuu vya umma vinapaswa kutafuta njia zenye ubunifu ili kuimarisha usalama wa kibaiolojia kutokana na ongezeko la tishio la usafirishaji usiodhibitiwa wa mada ya kibiolojia na kemikali za sumu.

Amesema Kenya ni kati ya nchi ambazo zimetia saini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kupiga marufuku utumizi wa mada za kibiolojia zinazoweza kuhatarisha amani ya dunia.
Naibu Kansela wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Jomo Kenyatta Mabel Imbuga amesema Kenya na nchi kadhaa za Afrika zinakabiliwa na hatari ya mada za kibiolojia na hivyo zinapswa kuwekeza katika miradi ya kukabiliana na changamoto hiyo.