Jan 18, 2018 07:11 UTC
  • 12 wauawa, 48 wajeruhiwa katika shambulio la Boko Haram nchini Nigeria

Watu 12 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulio la kujilipua kwa bomu lililotekelezwa sokoni katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tukio hilo lilijiri jana mchama katika eneo la Muna Garage ambayo ni kambi inayowahifadhi watu wasio na makazi nje ya makao makuu ya Maiduguri.

Wakimbizi katika kambi ya Muna Garage huko Miduguri 

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa wanawake wanne waliokuwa wamejifunga mabomu ndio waliotekeleza shambulio hilo. Hayo ni kwa mujibu wa Abdulkadir Ibrahim Msemaji wa Kitengo cha Taifa cha Huduma za Dharura cha Nigeria (NEMA).

Wakati huo huo shirika la habari la Nigeria limetangaza kuwa shambulio la jana lilifanywa na wanawake wawili waliokuwa wamejifunga mabomu na kusema kuwa watu 12 wameaga dunia na 48 wamejeruhiwa. Shambulio hilo la jana la kujilipua kwa bomu lililotekelezwa sokoni ni la kwanza kuwahi kutokea huko Maiduguri tangu kuanza mwaka huu wa 2018.  Pamoja na kuwa hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini kundi la Boko Haram ambalo lilianzisha mashambulizi huko kaskazini mashariki mwa Nigeria karibu muongo mmoja uliopita katika miaka ya hivi karibuni limekuwa likiilenga kambi ya Muna inayowahifadhi raia wasio na makazi.

 

Tags