Mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi wa vikosi vya ulinzi vya Niger
Rais wa Niger amefanya mabadiliko makubwa katika safu ya uongozi wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kwa shabaha ya kuimarisha vita dhidi ya ugaidi na kupambana na wanamgambo wenye misimamo ya kufurutu ada.
Kwa mujibu wa dikrii iliyotolewa na Rais Mahamadu Youssoufou wa Niger, Jenerali Ahmad Muhammad ameteuliwa kuwa kamanda mpya wa vikosi vya ulinzi huku Jenerali Ibraha Bolama Issa akiwa naibu wake. Wakati huo huo katika dikrii nyingine Rais wa Niger amewateua Naibu Mkuu wa vikosi vya nchi kavu pamoja na Kamanda Mkuu wa jeshi la polisi la nchi hiyo.
Mabadiliko hayo yamefanyika kufuatia ujumbe wa pongezi wa mwaka mpya uliotolewa na Rais wa Niger ambapo aliahidi kuviboresha vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo katika mwaka huu mpya wa 2018 na kukabiliana ipasavyo na vitisho vya kiusalama na kuzidisha mapambano dhidi ya wanamgambo wenye misimamo mikali na ugaidi.
Niger iko katika eneo linalokumbwa na machafuko la Ukanda wa Sahel na katika jangwa la Afrika ambayo katika miaka miwili ya hivi karibuni imeathiriwa na ukosefu wa amani na kuyumba kwa hali ya usalama kutokana na kuenea harakati za makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada. Kuwa karibu nchi hiyo na nchi kama Mali, Nigeria, Libya na Algeria kumeifanya nchi hiyo kukabiliwa na hatari kubwa. Kwa kadiri kwamba nchi hiyo ya eneo la Sahel barani Afrika katika miaka mitano ya hivi karibuni imekuwa mlengwa wa mashambulizi ya makundi yenye misimamo mikali na yale ya kigaidi yakiwemo mashambulizi ya kundi la Boko Haram kutokana na kuathiriwa na changamoto nyingi za kiusalama na khususan mgogoro wa kaskazini mwa Mali na vilevile mizozo ya silaha huko Libya.
Muhammad Ibn Chambas Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Magharibi mwa Afrika anasema kuwa: Vitendo vya mabavu, uchupaji mipaka na ugaidi vimesababisha migogoro mingi ya kibinadamu katika eneo la Sahel barani Afrika na kuutumbukia katika hatari kubwa umoja wa ardhi na kujitawala kwa nchi za eneo hilo.
Kuendelea mgogoro huko Libya na pia kushindwa kundi la kigaidi la Daesh huko magharibi mwa Asia na kuwepo uwezekano wa kuhama magaidi hao wananchama wa kundi hilo kuelekea Afrika yote hayo yamezidisha hatari ya kuenea ugaidi katika eneo hilo. Hali hiyo ya mambo imewapelekea viongozi wa Niger kuzingatia pakubwa suala la kuviboresha vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo. Wakati huohuo kuweko hatari ya kuenea ugaidi kumetoa msukumo kwa Marekani na waitifaki wake kuongeza idadi ya wanajeshi wao magharibi mwa Afrika. Hasa ikizingatiwa kuwa wanajeshi wa Marekani na Ufaransa wako katika eneo hilo kwa malengo maalumu na huku zikitilia maanani kudhamini maslahi yao na kunufaika na utajiri wa eneo hilo la Sahel barani Afrika lenye maliasili tajiri.
Licha ya juhudi zinazofanywa na viongozi wa Niger kwa ajili ya kuimarisha jeshi la nchi hiyo na kuwatolea wito nchi waitifaki wao kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi, lakini inaonekana kuwa mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel barani Afrika linahitajia marekebisho ya ndani na kuchukuliwa hatua kieneo na kimataifa mbali na hatua za kijeshi. Kuhusiana na suala hilo, katika upande wa ndani, hatua kama vita dhidi ya umaskini, kukosekana uadilifu, ufisadi na kutekelezwa jitihada za kutekeleza demokrasia; na katika uga wa nje masuala kama kuzidishwa ushirikiano wa kieneo kwa lengo la kuipatia ufumbuzi migogoro ya kisiasa huko Libya, kuandaliwa mazingira huko Mali na pia kuinuliwa kiwango cha ushirikiano wa kieneo katika nyanja mbalimbali yanapasa kupewa kipaumbele.