Uwanja wa ndege Libya wafunguliwa tena baada ya kujiri mapigano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39251-uwanja_wa_ndege_libya_wafunguliwa_tena_baada_ya_kujiri_mapigano
Uwanja wa ndege pekee uliokuwa ukifanya kazi huko Tripoli mji mkuu wa Libya ulifunguliwa tena jana Jumamosi baada ya kufungwa kwa siku tano kufuatia mapigano makali yaliyosababisha kuharibiwa ndege za abiria.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 20, 2018 23:40 UTC
  • Uwanja wa ndege Libya wafunguliwa tena baada ya kujiri mapigano

Uwanja wa ndege pekee uliokuwa ukifanya kazi huko Tripoli mji mkuu wa Libya ulifunguliwa tena jana Jumamosi baada ya kufungwa kwa siku tano kufuatia mapigano makali yaliyosababisha kuharibiwa ndege za abiria.

Uwanja wa ndege wa Mitiga unaopatikana mashariki mwa mji mkuu Tripoli jana ulionekana kurejea katika shughuli zake kama kawaida huku maeneo ya wanaowasili na kutoka yakiwa mashughuli na wasafiri.  Afisa mmoja katika uwanja huo wa ndege ameeleza kuwa ndege zote za ndani na kimataifa zimeanza kazi  na kwamba hakuna matatizo ya kiufundi au kiusalama yaliyoripotiwa hadi hiyo jana.  Mapigano ya Jumatatu iliyopita karibu na uwanja huo wa ndege wa Mitiga yalijiri kati ya kikosi maalumu cha ulinzi  katika uwanja wa ndege wa Mitiga chenye mfungamano na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayotambuliwa kimataifa na kundi la wanamgambo lenye makao yake katika wilaya ya Tajoura.

Watu wasiopungua 20 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika mapigano hayo. Libya imekuwa ikiathiriwa na mapigano kati ya makundi ya wanamgambo tangu nchi hiyo itumbukie katika hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani kufuatia kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.