Kuendelea operesheni za kijeshi nchini Libya dhidi ya makundi yenye silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39303-kuendelea_operesheni_za_kijeshi_nchini_libya_dhidi_ya_makundi_yenye_silaha
Mashambulizi ya jeshi la Libya dhidi ya makundi yenye silaha katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo yanaendelea kwa nguvu kubwa chini ya mwavuli wa operesheni ya "Ghadhabu ya Jangwani"
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 22, 2018 02:52 UTC
  • Kuendelea operesheni za kijeshi nchini Libya dhidi ya makundi yenye silaha

Mashambulizi ya jeshi la Libya dhidi ya makundi yenye silaha katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo yanaendelea kwa nguvu kubwa chini ya mwavuli wa operesheni ya "Ghadhabu ya Jangwani"

Mohammad al Manfour, ni mmoja wa makamanda wa kikosi cha anga cha Libya ambaye sambamba na kutangaza habari hiyo amesisitiza kuwa, ndege za kivita za Libya zinaendelea kufanya mashambulizi makali dhidi ya maficho ya makundi yenye silaha. Miongoni mwa malengo ya opeshenei ya Ghadhabu ya Jangwani ni kuyasafisha na kuyaangamiza kabisa makundi yanayofanya jinai ambayo yamejikita kusini mashariki mwa Libya na ambayo pia ni maarufu kwa kufanya mashambulizi ya holela na kuteka nyara raia.

Jeshi la Libya likisherehekea ushindi dhidi ya magaidi wa ISIS mjini Sirte

 

Kuzagaa magenge yenye silaha katika kona mbalimbali za Libya ni moja ya migogoro mikubwa ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Sehemu kubwa ya magenge hayo yana tabia ya kufanya mashambulizi ya holela na kuwateka nyara raia huku mengine yakijikita katika vitendo vya kigaidi na vya makundi ya wakufurishaji. 

Muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi NATO ndio unaobebeshwa lawama kubwa zaidi za kuivamia kijeshi Libya, kuyashehenesha silaha makundi hasimu na baadaye kuitelekeza nchi hiyo huku kila kundi likiwa limejizatiti kwa silaha nzito. Nchi za Magharibi zilitumia vibaya muundo wa kikabila wa Libya wakati wa kampeni za kuupindua utawala wa Kanali Muammar Gaddafi. Kwa kujua vyema muundo wa kiuhasama wa makabila ya Libya, nchi za Magharibi ziliivamia kijeshi Libya, zikavuruga vibaya mno miundombinu ya nchi hiyo na kuyapa nguvu za kijeshi makundi hasimu yenye mielekeo ya kikabila na baadaye kukaa pembeni na kuangalia kwa macho namna wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu wanavyomalizana wenyewe kwa wenyewe. Si hayo tu, lakini pia ripoti zinaonesha kuwa makundi mengi ya Libya yanaungwa mkono na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwa ni pamoja na kupelekewa kimagendo silaha na mahitaji yao yote ya kijeshi.

Salahuddin al Jamali, mjumbe wa Umoja wa Nchi za Kiarabu katika masuala ya Libya ameligusia suala hilo la kuingizwa kimagendo silaha nchini Libya na kusema kuwa, baadhi ya makundi yanaingiza silaha nchini Libya kiurahisi na kila siku kutoka nchi jirani hivyo haiwezekani kabisa kupatikana amani nchini humo katika mazingira kama haya. 

Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya

 

Kwa upande wake, Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema, kuna karibu silaha milioni 20 za aina mbalimbali nchini humo.

Mgogoro mwingine mkubwa wa Libya hivi sasa ni kuweko nchini humo magenge ya kigaidi. Hivi sasa makundi ya kigaidi yenye mfungamano na mtandao wa al Qaida, mabaki ya magaidi wa Daesh (ISIS) na wanamgambo wengine, wamejikita katika maeneo mbalimbali hususan ya kusini mwa Libya. Kukosekana serikali kuu yenye nguvu na kuendelea kuwepo mizozo ya kisiasa pamoja na kuingizwa kila siku silaha za magendo nchini Libya ni mambo ambayo yanalikwamisha jeshi la Libya katika vita vyake dhidi ya mkundi ya kigaidi. Pamoja na yote hayo, kuweko magenge ya kigaidi ndiyo hatari kubwa zaidi kwa Libya na dunia nzima kuliko hatari nyingine yoyote. 

Ahmad Qadhaf al Dam, mmoja wa viongozi wa zamani wa Libya amesema, kila siku mamia ya wanamgambo wa Daesh walioshindwa katika nchi za Syria na Iraq wanamiminika nchini Libya kwa ajili ya kuzusha machafuko nchini humo. 

Hivi sasa jeshi la Libya limeshadidisha mashambulizi yake kusini mwa nchi hiyo. Wanajeshi wa nchi hiyo wana matumaini kwamba watafanikiwa katika opereseheni zao za kuyasafisha magenge ya kigaidi na yenye silaha, iwapo juhudi zao hizo zitaendelea. Pamoja na hayo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, operesheni za kijeshi pekee hazitoshi kuangamiza magaidi hao, bali mafanikio ya operesheni hizo yanategemea nia ya kweli ya wanasiasa na wanajeshi sambamba na msaada wa kieneo na kimataifa kwa nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita.