Uchunguzi: Maelfu ya wanawake wanachama wa Daesh wako Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39381-uchunguzi_maelfu_ya_wanawake_wanachama_wa_daesh_wako_libya
Kituo kimoja cha utafiti cha Marekani kimeripoti kuwa, maelfu ya wanawake wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wako nchini Libya na kwamba 300 kati yao ni raia wa Tunisia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2018 11:31 UTC
  • Uchunguzi: Maelfu ya wanawake wanachama wa Daesh wako Libya

Kituo kimoja cha utafiti cha Marekani kimeripoti kuwa, maelfu ya wanawake wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wako nchini Libya na kwamba 300 kati yao ni raia wa Tunisia.

Kituo cha Utafiti cha Siasa za Mashariki ya Karibu cha Marekani mjini Washington kimetangaza kuwa, maelfu ya wanawake raia wa nchi za Tunisa, Australia, Ubelgiji, Ufaransa, Uingereza, Misri, Chad na nchi nyingine kadhaa za Afrika wamo kati ya magaidi wa kundi la Daesh nchini Libya. 

Matokeo ya uchunguzi wa kituo hicho yanasema kuwa, wanawake magaidi wa kundi la Daesh huko Libya wanafanya kazi zilezile walizokuwa wakifanya huko Iraq na Syria ikiwa ni pamoja na kuzaa watoto kwa wingi na kulea kizazi kipya cha magaidi wa kundi la Daesh.

Wapiganaji wa kike wa kundi la Daesh

Baada ya kupata vipigo mtawalia katika nchi za Iraq na Syria sasa kundi la kigaidi la Daesh linafanya mikakati ya kuimarisha nafasi yake katika nchi zenye machafuko na ukosefu wa usalama kama Libya na Afghanistan. 

Libya ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwaka 2011 baada ya Marekani na majeshi ya NATO kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya utawala wa zamani wa nchi hiyo.