Ikhwanul Muslimin ya Misri yatahadharisha kuhusu kuwekewa mashinikizo wapinzani
(last modified Fri, 26 Jan 2018 16:42:35 GMT )
Jan 26, 2018 16:42 UTC
  • Ikhwanul Muslimin ya Misri yatahadharisha kuhusu kuwekewa mashinikizo wapinzani

Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri imetahadharisha kuhusu hatua ya serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Abdel Fatah al Sisi ya kuwashinikiza wapinzani wa serikali na taathira zake mbaya za kisiasa.

Msemaji wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, Talaat Fahmy amaeashiria mashinikizo endelevu na makubwa yanayofanywa na serikali ya al Sisi dhidi ya wapinzani nchini Misri na kueleza kuwa, katika mazingira kama hayo wananchi wakataka tamaa na kupoteza matumaini au hata kulazimika  kutumia nguvu na silaha.  

Rais Abdel Fatah al Sisi wa Misri 

Fahmy ameongeza kuwa, kwa mtazamo wa Ikhwanul Muslimin, njia pekee ya kukomesha hali hiyo ni kurejeshwa uhuru na demokrasia nchini Misri.

Msemaji wa Ikhwanul Muslimin ameyatamka hayo baada ya Rais wa Misri, Abdel Fatah al Sisi kutangaza kuwa atagombea kiti cha rais wa nchi hiyo kwa mara ya pili. Wakati huo huo Sami Anan,  aliyetarajiwa kuwa mpinzani wa al Sisi katika uchaguzi ujao wa rais ametiwa mbaroni na jina lake limefutwa katika orodha ya wagombea wa kiti hicho.

Sami Anan, hasimu wa Rais wa Misri aliyetiwa mbaroni

Wagombea wengine kadhaa waliotazamiwa kuchuana na Generali Abdel Fattah al Sisi akiwemo Ahmad Shafiq Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo wametangaza kujitoa katika orodha ya wagombea wa kiti cha urais.

Uchaguzi wa Rais Misri umepangwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu. 

Tags