UN yashtushwa na kutapakaa maiti mashariki mwa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39589-un_yashtushwa_na_kutapakaa_maiti_mashariki_mwa_libya
Umoja wa Mataifa umeeleza wasi wasi wake kutokana na kutapakaa maiti za watu waliouawa katika mazingira ya kutatanisha mashariki mwa Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2018 04:41 UTC
  • UN yashtushwa na kutapakaa maiti mashariki mwa Libya

Umoja wa Mataifa umeeleza wasi wasi wake kutokana na kutapakaa maiti za watu waliouawa katika mazingira ya kutatanisha mashariki mwa Libya.

Taarifa ya Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL imesema maafisa wa UN wameshtushwa na habari za kupatikana miili mitano ya watu waliouawa katika kijiji cha Laithi mjini Benghazi, huku mitatu ikipatikana katika eneo la Derna, yapataka kilomita 250 mashariki mwa mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Libya.

UNSMIL imesema maiti za watu hao zina majeraha mengi yanayoonyesha kuwa waliteswa kabla ya kufyatuliwa risasi. Imeongeza kuwa, kufikia sasa haijabainika waliohusika na mauaji hayo.

Maafisa wa serikali wakifukua miili iliyofukiwa

Haya yanajiri siku chache baada ya watu wasiopungua 35 kuuawa na wengine 70 kujeruhiwa katika miripuko miwili ya mabomu iliyotokea mjini Benghazi. 

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011, kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato).