Zaidi ya wahajiri haramu 90 watoweka katika pwani ya Libya wakielekea Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39819-zaidi_ya_wahajiri_haramu_90_watoweka_katika_pwani_ya_libya_wakielekea_ulaya
Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limetangaza kuwa, makumi ya wahajiri haramu wametoweka katika maji ya pwani ya Libya baada ya boti yao kuzama baharini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2018 11:11 UTC
  • Zaidi ya wahajiri haramu 90 watoweka katika pwani ya Libya wakielekea Ulaya

Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limetangaza kuwa, makumi ya wahajiri haramu wametoweka katika maji ya pwani ya Libya baada ya boti yao kuzama baharini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Ijumaa ya leo, jumla ya wahajiri 90 wametoweka katika ajali hiyo huku watu watatu pekee wakiwa ndio waliofanikiwa kuokoka. Libya ni eneo kuu linalotumiwa na wahajiri wa Kiafrika katika njia yao ya kuelekea barani Ulaya. Magendo na biashara haramu ya binaadamu pia imeshamiri nchini Libya kutokana na ukosefu wa usalama, suala ambalo linapelekea kila mwaka maelfu ya wahajiri haramu kuingia Ulaya.

Miili ya wahajiri ikiopolewa kutoka baharini

Taarifa zaidi zinasema, kabla ya wahajiri hao kuanza safari huwa wanatoa kiwango kikubwa cha fedha kwa magenge yanayojishughulisha na magendo hayo kwa lengo la kuwafikisha eneo husika, ingawa wengi wao hupoteza maisha baharini kabla ya kufika waendako. Wimbi la wahajiri haramu kuelekea barani Ulaya, liliibuka kufuatia uingiliaji wa madola ya Magharibi ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika sambamba na kuuawa aliyekuwa kiongozi wake, Kanali Muammar Gaddafi. Mbali na matatizo ya raia wa Libya kukimbia nchi yao, wananchi hao hivi sasa wanateseka pia kwa ukosefu wa amani na uvamizi wa makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola hayo hayo ya Magharibi.