UN: Wafanya magendo ya binadamu Libya wanashirikiana na maafisa usalama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40087-un_wafanya_magendo_ya_binadamu_libya_wanashirikiana_na_maafisa_usalama
Ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyokabidhiwa Baraza la Usalama la umoja huo imefichua kuwa, wanaofanya magendo ya binadamu nchini Libya wana mafungamano na taasisi rasmi za usalama za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 08, 2018 10:20 UTC
  • UN: Wafanya magendo ya binadamu Libya wanashirikiana na maafisa usalama

Ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyokabidhiwa Baraza la Usalama la umoja huo imefichua kuwa, wanaofanya magendo ya binadamu nchini Libya wana mafungamano na taasisi rasmi za usalama za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Ripoti hiyo imesema makundi yanayobeba silaha na ambayo yamekuwa yakihusishwa na biashara hiyo ya utumwa nchini Libya yamekuwa yakipewa silaha na maagizo na maafisa wa taasisi za usalama nchini humo.

Hata hivyo Kikosi Maalumu cha Kupambana na Magendo ya Binadamu SDF kimepinga tuhuma hizo za wataalamu wa UN, na kusisitiza kuwa jukumu lake ni kukabiliana na wimbi la wahajiri haramu wanaoingia nchini humo kwa shabaha ya kutaka kupelekwa Ulaya, na tarayi kimeshakamata idadi kubwa ya wanaofanya magendo ya binadamu.

Hii ni katika hali ambayo, waraka wa siri uliokabidhiwa kwa wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita unasema kuwa, tangu wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh walipofukuzwa katika eneo la Sirte mwaka 2016, wamekuwa wakifanya jitihada za kuwa karibu zaidi na wafanya magendo ya binadamu nchini Libya. 

 

Wahajiri wa Kiafrika wanaouzwa kama watumwa nchini Libya

Ripoti hiyo ya siri yenye kurasa 157 inasema kuwa, magendo ya binadamu na ukiukaji wa haki za binadamu unaongezeka sana nchini Libya.

Wafanya magendo ya binadamu wamekuwa wakitumia hali ya ukosefu wa amani nchini Libya kwa ajili ya kusafirisha binadamu na kuwauza barani Ulaya na maeneo mengine ya dunia.