Wanachama wengine kadhaa wa Ikhwanul Muslimin wahukumiwa kifungo cha maisha jela Misri
(last modified Mon, 12 Feb 2018 04:36:00 GMT )
Feb 12, 2018 04:36 UTC
  • Wanachama wengine kadhaa wa Ikhwanul Muslimin wahukumiwa kifungo cha maisha jela Misri

Wanachama kadhaa wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin ya Misri wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya nchi hiyo.

Vyombo vya mahakama vya Misri vimetangaza kuwa mahakama ya mjini Cairo jana ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa wanachama wa wafuasi 17 wa Ikhwanul Muslimin, mbali na wengine 16 waliopewa adhabu ya vifungo vya miaka kadhaa jela.

Makumi ya wanachama na waungaji mkono wa harakati hiyo ya Kiislamu mnamo mwezi Machi mwaka 2014 waliandaa maandamano dhidi ya serikali katika eneo la A'inu-Shams mjini Cairo ambapo watu watatu waliuawa.

Muhammad Morsi, aliyekuwa rais wa Misri, ambaye naye pia amehukumiwa kifungo cha maisha jela

Mnamo mwaka huo Mkuu wa Mashtaka wa Serikali ya Misri aliwasilisha mashtaka dhidi ya watu 48 akidai kwamba walihusika na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubeba silaha na kuua.

Tangu Muhammad Morsi, rais aliyechaguliwa kidemokrasia, alipoondolewa madarakani mwaka 2013 kupitia mapinduzi ya kijeshi, harakati ya Ikhwanul Muslimin ambayo imepigwa marufuku na kutangazwa na serikali ya Misri kuwa ni kundi la kigaidi, imekuwa ikiandamwa na hatua kandamizi za serikali hiyo huku viongozi wake wengi waandamizi wakipewa adhabu mbalimbali na mahakama za nchi hiyo ikiwa ni pamoja na hukumu za vifo na vifungo vya maisha jela.../

Tags