Aliyeteka nyara ndege ya Misri ajisalimisha kwa polisi ya Cyprus
Wizara ya Mambo ya Nje ya Cyprus imesema kuwa, Seifuddin Mustafa, raia wa Misri aliyeteka nyara ndege ya abiria ya EgyptAir hatimaye amejisalimisha kwa vyombo vya usalama katika uwanja wa ndege wa Larnaca nchini Cyprus, baada ya masaa sita ya utekaji nyara.
Habari zinasema kuwa, mtekaji nyara huyo ambaye alikuwa amevaa fulana ya mada za miripuko ameonekana akitoka kwenye ndege ya EgyptAir yenye nambari MS181 akiwa ameweka mikono juu ishara ya kujisalimisha. Awali raia huyo wa Misri alikuwa ametoa masharti kadhaa kwa serikali ya Cairo na ile ya Cyprus. Seifuddin Mustafa alisema kuwa anaitaka serikali ya Misri iwaachie huru wafungwa wa kisiasa sawa na kusema kuwa anataka aletewe mtalaka wake raia wa Cyprus katika uwanja huo wa ndege waonane.
Kadhalika jamaa huyo anayeshukiwa kuwa na akili taahira alitoa masharti mapya kuwa anataka kukutana na kufanya mazungumzo na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya mbali na kuitaka serikali ya Cyprus kumpa hifadhi.
Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 55 na wahudumu 7 ilikuwa inatoka Alexandria kwenda jijini Cairo, kabla ya mtekaji nyara huyo kumuagiza rubani aigeuze na kuipeleka nchini Cyprus. Nicos Christodoulides, msemaji wa serikali ya Cyprus amesema kuwa utekaji nyara huo haukuwa wa kigaidi bali ni wa kisiasa na kwamba hakuna yeyote aliyeuawa au kupata majeraha mabaya mbali na mhudumu aliyepata majeraha madogo akiruka nje ya ndege hiyo kupitia dirishani akihofia usalama wake.