EU kupunguza ufadhili kwa askari wa Burundi walioko Somalia
Umoja wa Ulaya unapanga kupunguza ufadhili wake kwa askari wa Burundi ambao ni miongoni mwa wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM.
Duru za kidiplomasia zimearifu kuwa, mpango huo wa EU unanuia kuishinikiza serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kufanya mazungumzo na wapinzani ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa nchi hiyo ambao umesababisha mamia ya watu kupoteza maisha. Mwanadiplomasia wa EU ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, kuipunguzia Burundi ufadhili kwa askari wake walioko Somalia, kutaulazimisha Umoja wa Afrika kutafuta wafadhili mbadala na kwa msingi huo viongozi wa AU hawatakuwa na budi kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Burundi. Kwa sasa serikali ya Bujumbura ambayo ina askari 5,400 katika kikosi cha AMISOM, hupokea dola milioni 13 za Marekani kwa mwaka kutoka EU huku askari wake kwa jumla wakipokea dola milioni 52 kila mwaka. Mwanadiplomasia huyo amesema EU inafanya mazungumzo juu ya kufuta dola milioni 13 za Marekani ambazo serikali ya Burundi hupokea moja kwa moja kutoka umoja huo kila mwaka.
Nchi kadhaa za Ulaya tayari zimetangaza kukata misaada ya moja kwa moja kwa serikali ya Burundi. Machi 14, serikali ya Ubelgiji ilitangaza kuikatia Burundi misaada yake ya moja kwa moja ukiwemo mpango wa yuro milioni 432 za kufadhili miradi mbali mbali ya serikali, iliyoanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2014 na ilitazamiwa kumalizika mwaka 2020.
Hata hivyo Alain Nyamitwe, msemaji wa serikali ya Burundi alisema kuwa serikali ya Bujumbura haibabaishwi na kukatiwa misaada na ufadhili na nchi za Magharibi na kwamba mipango yake itaendelea kama kawaida.
Zaidi ya watu 400 wameripotiwa kuuawa hadi hivi sasa na karibu watu laki mbili na 40 elfu wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi, tangu Burundi ilipotumbukia kwenye machafuko yaliyotokana na Rais Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa muhula wa tatu.