Misri yaonya kuhusu hatari ya magaidi wa Daesh kuvamia kaskazini mwa Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameonya kuwa magaidi wa Daesh (ISIS) waliosafishwa huko Syria na Iraq wanafanya kila wawezalo kuzivamia nchi za kaskazini mwa Afrika hususan Libya.
Sameh Shoukry alisema hayo jana Ijumaa katika Mkutano wa Usalama wa Munich (MSC) huko Ujerumani na kuongeza kuwa, nchi zote duniani zinapaswa kuwa macho na kuchukua hatua za makusudi za kuzuia harakati mpya za magaidi wa Daesh ambao sasa wanavamia eneo la kaskazini mwa Afrika hususan Libya baada ya kushindwa katika nchi za Syria na Iraq.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameongeza kuwa, nchi yake ina wasiwasi mkubwa na hatari ya magaidi wa ISIS wanaokimbilia kaskazini mwa Afrika hasa Libya na katika eneo la Sahel linaloundwa na nchi za Mali, Niger, Mauritania, Chad na Burkina Faso baada ya magaidi hao kuangamizwa nchini Iraq na Syria.
Amesema kitendo cha magaidi hao kukimbia kutoka Iraq na Syria na kuelekea Libya na katika eneo la Sahel barani Afrika ni tishio kwa usalama na utulivu wa eneo hilo zima.
Mkutano wa Usalama wa Munich (MSC) ulianza jana Ijumaa huko Ujerumaini na kuhudhuriwa na viongozi wengi wa ngazi za juu wa nchi mbalimbali ulimwenguni. Mkutano huo unatarajiwa kuendelea na shughuli zake kadi kesho Jumapili.