Chaguzi ndogo zenye mchuano mkali zafanyika Tanzania
Habari kutoka nchini Tanzania zinasema kuwa zoezi kupiga kura katika chaguzi ndogo za ubunge na udiwani katika baadhi ya maeneo, Tanzania Bara limeanza rasmi asubuhi ya leo Jumamosi tarehe Februari 17, 2018.
Chaguzi hizo ni za ubunge katika majimbo mawili ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro chaguzi ambazo zimeitishwa baada ya kujiuzulu wabunge wa zamani wa majimbo hayo.
Chaguzi nyingine ni za madiwani wa kata nane Tanzania Bara. Zaidi ya wapiga kura laki 3 na 55,000 walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura wamepangia kutumia vituo 867 vya kupigia kura kuchagua wagombea wanaowapenda.
Vyombo vya habari vya Tanzania vimeripoti kuwa vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema leo asubuhi saa 2:00 na wananchi wamejitokeza kwa wingi katika mazingira ya ulinzi ulioimarishwa wa polisi.
Mchuano mkali uko katika jimbo la Kinondoni ambapo Said Mtulia wa CCM anachuana na Salum Mwalimu wa Chadema. Kwa upande wa jimbo la Siha huko Kilimanjaro, Elvis Christopher Mosi wa Chadema anachuana na Dkt. Godwin Ole Mollel wa CCM.
Katika tukio jingine, mawakala 67 kati ya 70 wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaosimamia uchaguzi mdogo Jimbo la Siha wametolewa vituoni kwa madai kuwa barua zao za kiapo zimesainiwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo pekee badala ya kusainiwa na hakimu.