Jeshi la Misri laua magaidi 7 wakufurishaji na kukamata wengine 408
Jeshi la Misri limetangaza kuwaaangamiza magaidi saba wakufurishaji katika oparesheni maalumu ya kijeshi inayoendelea katika eneo la Sinai nchini humo.
Msemaji wa Jeshi la Misri Kanali Tamer al-Rifai ametoa taarifa Jumamosi na kusema, katika siku ya tisa ya oparesheni ya wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo la Rasi ya Sinai, magaidi saba wakufurishaji wameuawa na washukiwa wengine 408 wa ugaidi kukamatwa.
Ameongeza kuwa, Jeshi la Misri limeharibu ngome kadhaa za magaidi tokea oparesheni hiyo ianze ambapo kwa ujumla magaidi 63 wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa. Tokea Februari 9 Jeshi la Misri lilianza kutekeleza oparesheni maalumu ya kuwatimua magaidi kutoka eneo la Rasi ya Sinai.
Magaidi wakufurishaji wenye itikadi za Kiwahabi, wakiwemo wafuasi wa kundi la ISIS, wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.
Shambulizi la hivi karibuni zaidi la matakfiri hao ni lile la mwezi Desemba katika Msikiti wa masufi wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini. Zaidi ya Waislamu 300 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala waliuawa katika shambulizi hilo.