Watu 61 wafariki dunia kwa homa ya uti wa mgongo nchini Niger
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa jumla ya kesi 736 za homa ya uti wa mgongo zimesajiliwa rasmi huko Niger mwaka huu, huku miongoni mwa kesi hizo watu 61 wakiripotiwa kuaga dunia kwa ugonjwa huo nchini humo.
Tawi la Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Niger imeeleza kuwa kesi hizo za homa ya uti wa mgongo (Meningitis) ziliripotiwa kati ya Januari 4 na Machi 13. Ofisi hiyo imeongeza kuwa watoto walio na umri wa chini ya miaka minne wanaunda asilimia 30 ya kesi hizo zilizotajwa huku asilimia 35 ya kesi za ugonjwa huo pia zikiwajumuisha watoto wenye umri kati ya miaka mitano na kumi na nne. Mwaka jana wa 2015 Niger iliathiriwa vikali na mlipuko wa homa ya uti wa mgongo uliosababishwa vifo vya watu 500. Mwezi Disemba mwaka jana Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitahadharisha kuhusu hatari ya kutokea milipuko mipya ya homa ya uti wa mgongo katika mwaka huu wa 2016 barani Afrika khususan huko Niger na Nigeria.