Kuna zaidi ya wahamiaji laki saba haramu huko Libya
Shirika la Kimataifa ya Wahajiri limesema kuwa, hivi sasa kuna zaidi ya wahamiaji haramu laki saba kutoka nchi 40 tofauti nchini Libya.
Kwa mujibu wa shirika hilo, sasa hivi kuna wahamiaji laki saba na nne kutoka nchi 40 tofauti wanaoishi kinyume cha sheria nchini Libya.
Ripoti ya shirika hilo inaonesha kuwa, asilimia 63 ya wahamiaji haramu walioko nchini Libya wanatoka katika nchi za Afrika zilizoko chini ya jangwa la Sahara, asilimia 29 wanatoka kaskazini mwa Afrika na asilimia nane wengine ni kutoka nchi za Mashariki ya Kati.
Shirika la Kimataifa la Wahajiri pia limesema, asilimia 22 ya wahajiri hao wanaoishi kinyume cha sheria nchini Libya wako katika mji mkuu Tripoli huku wahajiri 443 wakiwa wanashikiliwa katika korokoro au jela za Libya.
Libya ni njia kuu inayotumiwa na Waafrika wanaokimbilia maisha mazuri barani Ulaya. Wahajiri hao hulazimika kutoa fedha nyingi kwa magenge ya magendo ya binadamu na mara nyingi hawafiki waendako kwani imma wanaishia kwenye mikono ya magenge hatari na kupigwa mnada kama bidhaa sokoni au hupoteza maisha baharini wakati wanapotumia mitumbwi dhaifu sana kuvuka bahari ya Mediterranean kuelekea barani Ulaya.