HRW yaikosoa serikali ya Misri kwa ukandamizaji
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeikosoa serikali ya Misri kwa hatua yake ya kuwatia mbaroni kiholela wanasiasa wa upinzani nchini humo.
Shirika la Human Rights Watch jana lilitoa taarifa likiwakosoa viongozi wa Misri kwa hatua yao ya kuwatia mbaroni kiholela wanasiasa wa upande wa upinzani katika kukaribia uchaguzi wa rais nchini humo. Shirika hilo aidha limeitaka serikali ya Misri imwachie huru Abdel Moneim Aboul Fotouh mgombea wa zamani wa kiti cha urais na mkuu wa chama cha Misri Imara.
Taarifa ya Human Rights Watch imeongeza kuwa serikali ya Cairo inawakandamiza wapinzani kama stratejia kuu ya kuwalazimisha wapinzani na wakosoaji wa serikali hiyo kusalimu amri na kunyamaza kimya wakati huu wa kukaribia uchaguzi wa rais nchini. Nabil Sadegh Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Misri juzi Jumapili aliagiza kuzuiwa mali za Abdel Moneim Aboul Fotouh.
Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilidai kuwa, Aboul Fotouh alikamatwa kutokana na kuwa na uhusiano na kundi la Ikhwanul Muslimin na kupanga njama za kuchochea machafuko nchini Misri kwa kutumia anga ya hivi sasa ya uchaguzi wa rais. Uchaguzi wa tatu wa rais huko Misri baada ya kupinduliwa Husni Mubarak dikteta wa zamani wa nchi hiyo umepangwa kufanyika tarehe 26 na 28 Machi mwaka huu.