Serikali ya Kenya yaahidi kukomesha ugaidi unaovuruga elimu
Serikali ya Kenya imetangaza kuwa imebuni mpango ambao utahakikisha kwamba shughuli za masomo hazitaathiriwa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo hususan katika Kaunti ya Wajir kutokana na mashambulizi ya kigaidi ya kundi la al Shabab.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i amesema leo Jumatano kwamba wizara yake inashauriana na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba shughuli za masomo haziathiriwi na mashambulizi ya al Shabab.
Matiang'i amesema kuwa, serikali ya Nairobi imejitolea kikamilifu kulikabiliana na janga hili ili kuhakikisha haliwanyimi watoto haki ya kupata elimu.
Kauli hiyo imetolewa baada ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kutangaza kuwahamisha karibu walimu 200 kutoka kaunti hiyo.
Jumanne iliyopita mamia ya walimu wanaohudumu katika eneo hilo walikwenda katika ofisi za tume hiyo jijini Nairobi, wakitaka kuhamishwa, wakidai kuhangaishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wa eneo hilo.
Walimu wanaofunza katika kaunti hiyo pia wanataka kuhamishwa kutokana na mashambulio ya mara kwa mara ya wanamgambo wa kundi la Al Shabaab.
Wiki iliyopita, walimu watatu ambao si wenyeji waliuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la Al Shabaab.
Hadi kufikia Jumatatu iliyopita zaidi ya shule kumi zilikuwa zimefungwa katika eneo hilo, walimu wakilalama kwamba hawangeendelea kufanya kazi katika mazingira ambayo si salama.